MAZISHI YA ALBAN CHRISTOPHER KALEZA 31DEC2023

Поделиться
HTML-код
  • Опубликовано: 1 янв 2024
  • WASIFU WA MAREHEMU ALBAN CHRISTOPHER KALEZA
    UTANGULIZI:
    Wasifu wa marehemu Alban Christopher Kaleza ulioandaliwa na familia na kusomwa na Rev. Father Lucas Anthony Mussa, mwanafamilia, siku ya Jumapili tarehe 31 December 2023 katika Kanisa Kuu la Kristo, Mkunazini Zanzibar, kwenye Ibada ya Maziko. Alban Christopher Kaleza ni mtoto wa pili na pia wa mwisho wa Bwana Augustine Kaleza na Bibi Audrey Kaleza. Alizaliwa tarehe 19 February 1996 katika Hospitali ya Lugalo Dar es Salaam.
    ELIMU YAKE:
    Alianza Elimu ya Awali yaani (Nursery), kuanzia mwaka 2000 hadi 2003 katika Skuli ya St. Monica’s Mkunazini hapa Zanzibar. Alipata Elimu ya Msingi Mbarali Primary School mwaka 2004 hadi 2010, na Elimu ya Sekondari kidato cha I hadi cha III kuanzia mwaka 2011 mpaka mwaka 2013 Skuli ya Trifonia na kidato cha IV mwaka 2014 Skuli ya Higher Career.
    KOZI MBALIMBALI ALIZOFANYA:
    Alijiunga na kozi ya Usimamizi wa Hoteli yaani, (Hotel Management), Kituo cha Kanisa la Katoliki, Shangani Zanzibar mwaka 2016.
    Alisomea Kozi ya Teknolojia ya Habari yaani (Information Technology) katika Chuo cha Mwalimu Nyerere Foundation, Bububu Zanzibar.
    Pia Alban Christopher Kaleza alisomea Ufundi Umeme Chuo cha VETA Dar es Salaam.
    MAISHA YAKE
    Alban Christopher Kaleza alijitoa sana katika mambo ya kanisani, alikuwa mwanachama hai wa Jumuiya ya Vijana ya Kanisa, iitwayo Tanzania Anglican Youth Organization (TAYO). Alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu na Nahodha wa timu ya Kanisa Kuu la Kristo Mkunazini. Akiwa na timu hii ya kanisa na nahodha wa timu, Alban Kaleza amefanikiwa kuchukua Ubingwa wa Makombe ya TAYO ya Mpira wa Miguu mara mbili huko Dodoma, na September 2023 pia alifanikisha kuchukua ubingwa huko Mbeya. Aidha mbali na kuchezea timu ya kanisani, pia alikuwa mchezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Wasambaa ya Mbweni na Timu ya Stoke City ya Mwera Mtofaani hapa Zanzibar. Na kwa upande wa huduma katika kanisa, Alban Kaleza alikuwa mhudumu wa madhabahuni. Vijana wengi wa umri wake katika Kanisa la Mkunazini huacha kuhudumia madhabahuni, lakini Alban Kaleza aliendelea kuhudumu madhabahuni akishika Chetezo, Msalaba au akiwa MC, aliendelea hudumia mpaka kifo kilipomkuta.
    UGONJWA
    Jumapili tarehe 17/12/2023 hakuwa amejisikia vizuri, na ingawa alicheza mechi ya Mpira wa miguu, lakini afya ya Alban Christopher Kaleza ilianza kuzorota, na ilipofika tarehe 21/12/2023 alipelekwa Kituo cha Afya Chukwani na kuchukuliwa vipimo, na kuonekana kuwa ana Malaria Kali.
    Tarehe 23/12/2023 hali yake ilizidi kudhoofika na kupelekwa katika Hospitali ya KMKM Kibweni kwa matibabu zaidi.
    Lakini tarehe 24/12/2023 alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja na kulazwa katika Wodi ya Wanaume. Jioni ya siku hiyohiyo hali ilizidi kuwa mbaya na kuhamishiwa Kitengo cha Uangalizi Maalumu (ICU).
    Tarehe 26/12/2023 saa 6.00 usiku hali ya Alban ikawa mbaya zaidi kiasi kwamba waliitwa mapadre, Canon Emmanuel Masoud na Fr. Godwin Masoud ambao walifika kumfanyia sala fupi na kumpaka Mafuta Matakatifu kama ilivyo desturi ya Sakramenti hiyo.
    KIFO CHAKE
    Siku ya Ijumaa tarehe 29/12/2023 Alban Kaleza aliamka vizuri na kufanyiwa usafi, kubadilishwa nguo zake na kurudishwa kitandani kwake ili kupata kifungua kinywa. Baada ya kula machungwa mawili, hali ikabadilika ghafula na alishindwa kabisa kunywa supu aliyoandaliwa, na alianza kulalamika maumivu ya tumbo, mgongo na kiuno. Madaktari walifika na walijitahidi sana kumshughulikia lakini ilipofika saa 1.30 asubuhi Alban alifariki dunia. Alban amewaacha baba na mama yake mzazi, na kaka yake wa pekee.
    SHUKRANI
    Familia ya Marehemu Alban Kaleza inawashukuru kwa dhati Canon Emmanuel Masoud na Fr. Godwin Masoud kwa huduma za kiroho. Familia pia inawashukuru Vijana na uongozi wa TAYO wa Mtaa wa Kanisa Kuu la Kristo, Mkunazini. Vilevile, inawashukuru wahudumu wote waliofika kutaka kufanya sala, ingawa hawakupata nafasi hiyo. Aidha familia inawashukuru madaktari na wauguzi wa Kituo cha Afya cha Chukwani na Hospitali ya KMKM Kibweni. Na hasa tunawashukuru madaktari na wauguzi wa Kitengo cha ICU cha Hospitali ya Rufaa ya Mnazi-mmoja kwa jitihada zao. Inawashukuru ndugu, jamaa, majirani na marafiki wote, na kila mmoja aliyeshirikiana nasi wakati wa ugonjwa wa Alban na wakati huu wa msiba na kwa misaada na michango mbalimbali ya hali na mali waliyotoa.
    Familia itaendelea kumkumbuka sana Alban Christopher Kaleza kwa upole wake, utulivu, ucheshi na upendo wake kwa kanisa na kwa watu wote. Familia inapenda kuhitimisha wasifu huu kwa kunukuu maneno ya Biblia kutoka Wafilipi 3:20-21; Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.

Комментарии • 6